Monday, May 22, 2017

Trump azuru Israel chini ya ulinzi mkali

Donald Trump (kushoto) na Benjamin Netanyahu wakiwa na wake zao uwanja wa ndege wa Tel Aviv        
Rais wa Marekani Donald Trump amewasili nchini Israel akiendelea na ziara yake ya kikazi katika maeneo ya Mashariki ya Kati ambapo pia anatarajiwa kuzuru Maeneo ya Wapalestina.
Amefika huko akitokea Saudi Arabia, mshirika muhimu wa Marekani, ambako alitoa hotuba katika mkutano mkuu wa nchi za Kiarabu na Kiislamu.
Bw Trump anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Israel na Palestina katika kipindi cha siku mbili atakazokuwa eneo hilo.
Rais huyo amesema kupatikana kwa mkataba wa amani kati ya Waisraeli na Wapalestina yatakuwa mafanikio makubwa, lakini hakusema mkataba kama huo unafaa kuchukua mwelekeo gani.
Amesema angependa sana pande zote mbili ziamue kuhusu mkataba huo wa amana kwa mashauriano ya moja kwa moja.
Katika mkutano mkuu wa viongozi wa Kiislamu na Kiarabu mjini Rihadh siku ya Jumapili, Bw Trump aliwataka viongozi hao kuwa kwenye mstari wa mbele katika kukabiliana na wanamgambo wa Kiislamu na wapiganaji wenye itikadi kali na "kuwafurusha kutoka kwenye dunia hii."
Aliitaja moja kwa moja Iran na kusema kwamba imekuwa "ikichochea mizozo ya kidini na ugaidi" katika kanda hiyo kwa miongo mingi.
Bw Trump pia alikariri tena kwamba anaamini amani kati ya Waisraeli na Wapalestina inaweza kupatikana.
Rais huyo wa Marekani amekuwa akichukuliwa sana kuwa muungaji mkono mkubwa wa Israel kuliko mtangulizi wake Barack Obama.
Amechukua msimamo usio mkali kuhusu suala tata la Israel kujenga makazi ya walowezi maeneo ya Wapalestina na kudokeza kwamba upanuzi wa makao hayo na si kuwepo kwa makao yenyewe, unaweza kuwa ndio kikwazo katika kutafuta amani.
Zaidi ya Wayahudi 600,000 huishi katika makao makazi 140 ya walowezi ambayo yamejengwa tangu Israel ilipotwaa maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Mashariki mwa Jerusalem mwaka 1967, maeneo ambayo Wapalestina huyachukuliwa kuwa sehemu ya "taifa litakaloundwa" la Wapalestina.