 |
Donald Trump (kushoto) na Benjamin Netanyahu wakiwa na wake zao uwanja wa ndege wa Tel Aviv | | | | | | | |
Rais wa Marekani Donald Trump
amewasili nchini Israel akiendelea na ziara yake ya kikazi katika maeneo
ya Mashariki ya Kati ambapo pia anatarajiwa kuzuru Maeneo ya
Wapalestina.
Amefika huko akitokea Saudi Arabia, mshirika muhimu
wa Marekani, ambako alitoa hotuba katika mkutano mkuu wa nchi za Kiarabu
na Kiislamu.
Bw Trump anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Israel na Palestina katika kipindi cha siku mbili atakazokuwa eneo hilo.
Rais
huyo amesema kupatikana kwa mkataba wa amani kati ya Waisraeli na
Wapalestina yatakuwa mafanikio makubwa, lakini hakusema mkataba kama huo
unafaa kuchukua mwelekeo gani.
Amesema angependa sana pande zote mbili ziamue kuhusu mkataba huo wa amana kwa mashauriano ya moja kwa moja.
Katika
mkutano mkuu wa viongozi wa Kiislamu na Kiarabu mjini Rihadh siku ya
Jumapili, Bw Trump aliwataka viongozi hao kuwa kwenye mstari wa mbele
katika kukabiliana na wanamgambo wa Kiislamu na wapiganaji wenye itikadi
kali na "kuwafurusha kutoka kwenye dunia hii."
Aliitaja moja kwa moja Iran na kusema kwamba imekuwa "ikichochea mizozo ya kidini na ugaidi" katika kanda hiyo kwa miongo mingi.
Bw Trump pia alikariri tena kwamba anaamini amani kati ya Waisraeli na Wapalestina inaweza kupatikana.
Rais huyo wa Marekani amekuwa akichukuliwa sana kuwa muungaji mkono mkubwa wa Israel kuliko mtangulizi wake Barack Obama.
Amechukua
msimamo usio mkali kuhusu suala tata la Israel kujenga makazi ya
walowezi maeneo ya Wapalestina na kudokeza kwamba upanuzi wa makao hayo
na si kuwepo kwa makao yenyewe, unaweza kuwa ndio kikwazo katika
kutafuta amani.
Zaidi ya Wayahudi 600,000 huishi katika makao
makazi 140 ya walowezi ambayo yamejengwa tangu Israel ilipotwaa maeneo
ya Ukingo wa Magharibi na Mashariki mwa Jerusalem mwaka 1967, maeneo
ambayo Wapalestina huyachukuliwa kuwa sehemu ya "taifa litakaloundwa" la
Wapalestina.